Aliyekua kiungo wa klabu za FC Barcelona, Inter na Paris Saint-Germain Thiago Motta amekabidhiwa mikoba ya kuwa mkuu wa benchi la ufundi la Genoa, akichukua nafasi ya Aurelio Andreazzoli.
Andreazzoli alifutwa kazi jana Jumanne, kufuatia kuandamwa na matokeo mabaya kwa muda wa miezi minne, na kuifanya klabu ya Genoa kuendelea kuwa nafasi ya pili kutoka mkiani mwa msimamo wa ligi ya Italia (Serie A).
Hii ni mara ya kwanza kwa Motta kuchukua jukumu la kuongoza kikosi kinachoshiriki ligi kubwa, na mara ya mwisho alikua kocha wa kikosi cha vijana chini ya umri wa miaka 19 cha Paris Saint-Germain.
Gwiji huyo mwenye umri wa miaka 37, alitangaza kustaafu soka mwaka 2018, na aliwahi kuitumikia klabu ya Genoa katika michezo 27, msimu wa 2008-09.
Mtihani wa kwanza wa Motta, utakua mwishonji mwa juma hili, ambapo kikosi chake kitashuka dimbani kupambana dhidi ya Brescia, katika mshike mshike wa ligi kuu ya soka nchini Italia (Serie A).