Klabu ya Chelsea inajipanga kumsajili kwa mara ya pili mlinda mlango kutoka Jamuhuri ya Czech Petr Cech, baada ya kumuuza kwa majirani zao Arsenal miaka mitatu iliyopita.
Chelsea wameibuka na mpango huo, kufuatia mlinda mlango wao kutoka nchini Ubelgiji Thibaut Courtois kuwa mbioni kujiunga na mabingwa wa soka barani Ulaya Real Madrid.
Courtois kwa sasa yupo mapumzikoni mjini Tenerife nchini Hispania, baada ya kumaliza majukumu ya kuitumikia timu yake ya taifa ya Ubelgiji iliyomaliza katika nafasi ya tatu, kwenye fainali za kombe la dunia.
Mbali na mkongwe huyo, wababe hao wa Stamford Bridge pia wanamfikiria mlinda mlango wa Leicester City Kasper Schmeichel ama Gianluigi Donnarumma wa AC Milan ya Italia.
Tayari Arsenal wameshaweka wazi suala la kumuweka sokoni Cech, baada ya meneja wa klabu hiyo Unai Emery kumsajili mlanda mlango kutoka nchini Ujerumani Bernd Leno aliyekua mtumishi wa klabu ya Bayer Leverkusen tangu mwaka 2011.
Emery anahitaji kufanya biashara ya kumuuza Cech, ili apate fedha zitakazo muwezesha kumsajili kiungo kutoka nchini Ufaransa na klabu ya Sevilla CF Steven N’Zonzi, ambaye mwishoni mwa juma lililopita alijumuika na wachezaji wenzake kusheherekea ubingwa wa kombe la dunia.
Hata hivyo mlinda mlango huyo tayari ameshakataa kuondoka klabuni hapo baada ya kutumwa ofa kutoka SSC Napoli ya Italia, na badala yake amesisitiza yupo tayari kugombania nafasi katika kikosi cha kwanza dhidi ya Bernd Leno.