Beki kutoka nchini Rwanda Thierry Manzi amefunguka kwa mara ya kwanza kuhusu mpango wa kuwindwa na Klabu ya Simba SC, ambayo imedhamiria kukisuka upya kikosi chake kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ na Michuano ya Kimataifa inayoratibiwa na CAF.
Manzi kwa sasa yupo nchini Ubelgiji alikokwenda katika mazungumzo na baadhi ya timu za huko ili kumsajili, lakini Simba SC tayari imeonyesha nia ya kumuhitaji na imeanza kumshawishi ikimtaka arudi Dar es Salaam wazungumze na kusaini kama kila kitu kitakwenda sawa.
Manzi amesema suala la kuhusishwa na Simba SC hawezi kulikataa ama kulikubali kwa sasa, lakini amekiri lolote linaweza kutokea kutokana na kipindi hiki ambacho klabu nyingi duniani zimeanza kujiandaa kufanya usajili.
Hata hivyo Beki huyo ambaye aliwahi kucheza Ryon Sport chini na Kocha Robertinho amesema kwa sasa hawezi kuzungumzia kwa undani suala la usajili na anasubiri muda utaongea, ingawa dili zipo nyingi.
“Ni kipindi cha usajili hivyo kama umefanya vizuri basi lazima utaongelewa, sijakubali wala kukataa habari hizo za Simba SC lakini jibu la mwisho ni muda. Nadhani tuwe wavumilivu na muda ukifika itafahamika wapi nitasaini ingawa dili zipo nyingi sana,” amesema Manzi
Manzi kwa sasa ni miongoni mwa mabeki wa kati walio kwenye kiwango bora akiwa ameisaidia AS Kigali kukaa nafasi ya nne kwenye msimamo huku akihusika katika mechi zote za Amavubi ilizocheza hivi karibuni zikiwemo zile za kuwania kufuzu fainali za mataifa ya Afrika (AFCON).
Manzi ni beki wa kati anayemudu kucheza namba nne na tano akitumia vyema miguu yote kwa ufasaha na anasifika kwa kukaba, kuanzisha mashambulizi, matumizi ya nguvu na ni mkali wa kucheza mipira ya juu.
Mbali na Rayon Sports, Manzi amewahi kucheza soka nchini Georgia katika klabu ya FC Dila Gori inayoshiriki Ligi Kuu ya huko, FAR Rabat ya Morocco na AS Kigali ya nchini kwao Rwanda.