Mbunge wa Muleba Kusini, Profesa Anna Tibaijuka amefafanua kauli yake tata iliyozua gumzo, kufuatia mgao wa Sh.1.6 bilioni aliopewa na mmiliki wa kampuni ya VIP Engineering and Marketing, James Rugemalira zilizoelezwa kuwa ni fedha za ufisadi zilizovunwa kupitia akaunti ya Tegeta Escrow.
Fedha hizo ni kati ya Sh.306 bilioni zilizoondolewa kinyamela kwenye akaunti ya Tegeta Escrow mwaka 2014.
Profesa Tibaijuka ambaye wakati huo alikuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi alibainika kuwa ni mmoja kati ya watu waliopokea mgao uliotokana mabilioni ya fedha zilizokuwa kwenye akaunti ya Tegeta Escrow zilizotolewa kimakosa na kupewa kampuni ya IPTL wakati mgogoro wa fedha hizo kati ya kampuni hiyo na Tanesco haujamalizika, na fedha hizo hazikutakiwa kuchukuliwa hadi mahakama itakapoamua ni za nani kati ya Tanesco (Serikali) au kampuni ya kufua umeme ya IPTL.
Rais wa awamu ya nne, Dkt. Jakaya Kikwete alitengua uteuzi wa Tibaijuka akieleza kuwa alipokea fedha hizo kupitia akaunti yake binafsi ingawa alidai alipewa kama msaada wa shule zake.
Hata hivyo, kauli zote za Tibaijuka kukana kuwa na hatia katika sakata hilo hazikuchukuliwa kwa uzito, hadi alipotoa kauli moja mbele ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, aliposema kati ya fedha hizo “Sh.10 milioni zilikuwa fedha za Mboga.”
Akizungumza hivi karibuni na Millard Ayo jijini Dodoma, Profesa Tibaijuka alieleza kuwa kauli hiyo ilitokana na tafsiri ya kabila lake la Kihaya.
“Kwanza sijawahi… na huwezi ukaleta clip inayosema mimi nilisema bilioni 1 (bilioni 1.9) ni pesa ya mboga. Mimi nilikuwa ninamjibu mwanasheria wa serikali nikiwa nimeshtakiwa katika mahakama ya maadili, kwamba nimepewa fedha na ndugu yangu Rugemarila,”
“Sasa yule alikuwa na benki statement yangu akaniuliza, maana yake alisema hizi milioni kumi zilikuwa za nini? Sasa kwa Kiswahili changu cha kihaya nilitakiwa kusema ‘ni fedha za matumizi yangu binafsi’, lakini sisi wahaya huwa tunazungumza kwa Kihaya huwa tunazungumza kwa kejeli… na ndio maana kule jimboni haijaniletea shida hata kidogo, maana walielewa pesa ya mboga maana yake ni matumizi ya kwangu binafsi,”
Alidai kuwa ingawa alijieleza kwa lugha hiyo, walikuwa wamenunuliwa waandishi kwa ajili ya kumchafua ili kumfanya ashindwe ubunge lakini bado alifanikiwa kuchaguliwa tena.
Wakati huo, Kamati ya Bunge ilieleza kuwa imebaini fedha za akaunti ya Tegeta Escrow zilichukuliwa benki kwa kutumia magunia na kwamba mgao wake uligusa viongozi wa kisiasa na wakidini.
Sakata hilo lilisababisha bunge kupendekeza aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Francis Werema pamoja Bodi ya Wakurugenzi ya Tanesco kuondolewa mara moja. Pia, ilipendekeza Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kutumbuliwa. Mapendekezo hayo yalifikiwa baada ya viongozi hao kung’oka mmoja baada ya mwingine.