Shirikisho la soka duniani (FIFA) limesema hadi sasa limeshauza jumla ya tiketi 742,760 za kutazama michuano ya kombe la dunia mwakani nchini Urusi, katika awamu ya kwanza ya mauzo ya tiketi hizo.
Kwa mujibu wa taarifa ya FIFA, asilimia 47 ya maombi yote yanatoka kwa wenyeji Urusi, na asilimia 53 ndiyo yanatoka kwenye mataifa mengine huku droo ya mwisho ya uuzaji wa tiketi katika awamu hiyo ikitarajiwa kufanyika Ijumaa wiki hii.
Miongoni mwa mataifa kumi yanayoongoza kwa maombi mbali na Urusi ni pamoja na Marekani, Brazil, Ujerumani, China, Mexico, Israel, Argentina, Australia na England.
Bei ya tiketi hizo ni kati ya pauni 79 (TZS 240,000/-) kwa ajili ya mechi za raundi ya pili ya hatua ya makundi hadi pauni 829 (TZS milioni 2.5) kwa ajili ya kutazama mchezo wa fainali.
Jumla ya tiketi milioni 2.5 zimeandaliwa kwa ajili ya kutazama mechi zote 64 zitakazopigwa katika viwanja 12 tofauti vilivyo katika majiji 11 ya Urusi.
Awamu ya pili ya mauzo inatarajiwa kuanza Desemba 5, mwaka huu na kuhitimishwa Januari 31, mwakani.