Ili kuendeleza soko la Bima kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu Mamlaka ya usimamizi wa Bima Tanzania – TIRA na Bodi ya Taifa ya Bima wanampango wa miaka Mitano wa Maendeleo ya Taifa (FYDPII-2020-2025), wa kuweka mazingira wezeshi ya Sekta ya Bima kwa minajili ya kuwa na soko lisilokuwa na udanganyifu, lenye ushindani, weledi na litakaloleta faida.
Kamishina wa Bima, Dkt. Baghayo Saqware ameyasema hayo katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, na kudai kuwa baadhi ya mipango ijayo ya Mamlaka ni pamoja na Kuanzisha na kutekeleza Mpango wa kitaifa wa Bima ya Kilimo, Uanzishwaji wa bodi ya wataalamu wa Bima, Hifadhi ya Jamii na Takwimu Bima, Kuunganisha mifumo ya kidigitali na Taasisi mbalimbali za umma ikiwemo Jeshi la Polisi, LATRA, NIDA, TASAC, TRA, PTA na ZRA.
Amesema, “mpango mkuu wa Taifa ni wa kuendeleza Sekta ya Fedha Nchini (FSDMP2020-2030), kupitia Ilani ya Chama cha Mapinduzi (2020-2025), Sera ya Uchumi wa Buluu Zanzibar, Maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan wakati akilihutubia Bunge April 2021, maelekezo ya Rais Dkt. Mwinyi wakati wa Ufunguzi wa Mkutano wa Wakuu wa Taasisi za Bima Septemba 2022 na Maelekezo ya Spika wa Bunge Novemba 2022 wakati wa semina ya Elimu ya Bima na Usalama Barabarani kwa Wabunge.”
Aidha, Dkt. Saqware amesema, Mamlaka inaendelea na mkakati wake wa utoaji wa elimu kwa umma kwa kushirikisha wadau wote kwenye sekta, ikilenga kufikia asilimia 80 ya watanzania wote wenye umri wa miaka zaidi ya 18 ifikapo mwaka 2030 na utoaji elimu ya bima na uhamasishaji wa Serikali, Idara, Taasisi za Umma.
“Elimu hii itasaidia kuzingatia Sheria ya Bima Sura 394, kif.133 (1)hadi(3), kif.140 na Sheria ya Umma Na. 7 ya Mwaka 2011, kif. 4 (2) (b). Hadi mwezi Julai 2023, Mamlaka imezitembelea Wizara za Kilimo; Wizara ya Nishati na Wizara ya Uchukuzi na Ujenzi na TAMISEMI. Mkakati huu ni endelevu na utazifikia Wizara, Idara na Taasisi mbalimbali za Umma,” alisema.
Aidha Saqware ameongeza kuwa, “kulinda haki za mteja wa Bima, Mamlaka imeendelea kuzisimamia kampuni za bima kuhakikisha zinalipa madai na fidia stahiki kwa wakati na kwa haki. Hadi sasa ulipaji wa madai na fidia stahiki kwa wateja wabima yamefikia asilimia 95 hivyo kupungua kwa malalamiko, hata hivyo asilimia 5 ya madai na fidia yana changamoto ambazo TIRA inafuatilia na kutoa suluhisho.”
TIRA, ni mamlaka iliyoanzishwa kwa Sheria ya Bima ya mwaka 2009 Sura Na.h 394 ikiwa na majukumu ya kusajili na kutoa leseni kwa watoa huduma za bima; kuandaa na kutoa kanuni na miongozo mbalimbali ya kusimamia soko la bima na Kurekebisha Sheria, kutoa elimu ya bima kwa umma, kulinda haki za mteja wa Bima na kushauri Serikali kuhusu mambo ya Bima.