Wakazi mkoani Kagera wanaoishi mabondeni wametakiwa kuchukua tahadhari kutokana na utabiri uliofanywa na Mamlaka ya hali ya hewa nchini TMA kuonyesha kuendelea kuwepo kwa mvua kubwa zinazotarajia kunyesha mkoani humo.
Tahadhari hiyo imetolewa na Meneja wa mamlaka ya hali ya hewa mkoani Kagera, Steven Marundo ambapo amesema kuwa kihistoria mkoa wa Kagera hasa manispaa ya Bukoba imekuwa ikipata mvua nyingi na kubwa zinazosababisha madhara kwa msimu wa masika zinazotokea mwishoni mwa mwezi Aprili hadi Mei.
Amesema kuwa utabiri uliofanywa na mamlaka hiyo unaonyesha kuwepo kwa mabadiliko tofauti na utabiri wa awali ambapo mvua zilitarajiwa kukoma mwezi Mei mwishoni lakini utabiri umeonyesha kuendelea kunyesha kwa mvua hadi katikati ya mwezi June na kuwataka wananchi wachukue tahadhari.
Aidha, Marundo amesema kuwa mkoa wa Kagera unapata mvua zake nyingi kutoka katika misitu ya Congo ambayo mwaka huu imekuwa na kiwango cha mililita 110 na kusababisha ardhi kujaa maji na kuongeza kuwa kwa mwaka 2016 ilinyesha mvua yenye ukubwa wa mililita 106.
Hata hivyo, ameongeza kuwa mvua kubwa kutokea kunyesha mkoani Kagera imenyesha mwaka 1994 ambapo mvua hiyo ilikuwa na ukubwa mililita 248 na kusababisha madhara makubwa mkoani humo,