Meya wa Manispaa ya Ubungo kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Boniface Jacob amesema kuwa chama hicho kwasasa kimetoa ruhusa ya kuwapokea baadhi ya waliokuwa wanachama na viongozi wake ambao walikihama chama hicho kuelekea vyama vingine ikiwemo CCM.

Ameyasema hayo jijini Dar es salaam alipokuwa akimpokea kada wa Chama Cha Mapinduzi, Gonga Kidera ambaye zamani alishawahi kuwa kiongozi ndani ya CHADEMA, lakini alihamia CCM ili kumuunga mkono Rais Magufuli.

”Mwanzoni chama kilikataa lakini sasa hivi kimekubali, ndiyo maana mnamuona Kidera sasa hivi yuko hapa, huyu ni moto ametoka CCM asubuhi na sasa hivi amejiunga na chama chake cha zamani, Sio huyu tu yupo jamaa mmoja alishawahi kuwa kiongozi wa chama fulani cha upinzani akahamia CCM, baada ya kuridhishwa na kazi nzuri ya Rais Magufuli, huyu ambaye simtaji lakini ametufuata akituomba ushauri baada ya kuona chama chake cha zamani hakieleweki tukamwambia aje hatuna tatizo naye muda ukifika nitamtaja.”amesema Jacob .

Hata hivyo, mara ya mwisho mwanasiasa maarufu ambaye alifanikiwa kujiunga na chama hicho ni aliyekuwa Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu ambaye alijiunga Novemba 19, 2017, kwa kile alichodai kuwa ni kutokuwepo kwa demokrasia ndani ya CCM.

Muhimu: Fahamu kiundani kansa ya tezi dume, dalili na visababishi vyake
TMA yawatahadharisha wakazi wa Kagera