Rais wa Togo Faure Gnassingbe ametoa taarifa kuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo ya Afrika Magharibi Komi Selom Klassou na serikali yake wamejiuzulu.
Katika taarifa hiyo kupitia wavuti wake rasmi, rais Gnassingbe amempongeza Klassou na mawaziri wake kwa juhudi zao za kiuchumi, kisiasa na kijamii pamoja na na matokeo ya kutia moyo licha ya janga la kiafya linaloikumba dunia.
Togo ilikuwa ifanyiwe mabadiliko ya kisiasa tangu Gnassingbe alipochaguliwa tena mnamo Februari kwa muhula wa nne ofisini, lakini mabadiliko hayo yalicheleweshwa kutokana na janga la virusi vya corona.
Ushindi wa uchaguzi wa rais, ambao ulikuja baada ya mabadiliko ya katiba kumruhusu Gnassingbe agombee, ulirefusha utawala wa familia ya Gnassimgbe kwa zaidi ya nusu karne.
Klassou mwenye umri wa miaka 60 amewahi kuhudumu kama waziri wa utamaduni, vijana na michezo na baadaye waziri wa elimu kabla ya kuteuliwa kama waziri mkuu wa Togo, nafasi ambayo amehudumu tangu mwaka 2015.