Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete amewaagiza Maafisa Utumishi wa Halmashauri zote nchini kuacha tabia ya kukaa ofisini badala yake watembelee ofisi za Watumishi zilizopo katika Kata na Vijiji ili kutatua changamoto za watumishi walioko huko.
Kikwete ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, ikiwa ni siku yake ya tatu ya ziara anayoendelea kufanya mkoani Mara ambapo amewataka Maafisa Utumishi hao kuleta matumaini kwa Watumishi wenzao.
“Katika ziara zenu mtakazojipangia za kutembelea vituo vya kazi hakikisheni mnatatua changamoto za watumishi wenu huku mkitumia nafasi hizo kwa kuwapatia taarifa za fursa mbalimbali za kiuchumi na za kujiendeleza kielimu zinazopatikana kwa sasa ” amesema Kikwete.
Aidha, amepiga marufuku tabia ya baadhi ya Maafisa Utumishi kutoa vibali vya kusafiri kwa Watumishi kwenda Jijini Dodoma katika Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa ajili ya kufuatilia masuala yao binafsi ya kiutumishi ilhali kazi hiyo ni ya Maafisa Utumishi hao.
Amesema, Watumishi hao hufika Dodoma kwa ajili ya kufuatilia kupandishwa madaraja, kubadilishiwa miundo na kada, kudai malimbikizo ya mshahara, kuwa vitendo hivyo vinawanyima fursa wananchi kuhudumiwa na Watumishi hao waliolazimika kusafiri.
Hata hivyo, amewaeleza Maafisa Utumishi hao ni lazima wahakikishe utendaji kazi zao unakuwa wa kimkakati na sio kufanya kazi kwa mazoea ba kusema moja ya jukumu la msingi kwa Maafisa Utumishi ni kuhakikisha Watumishi wanaowaongoza wanatatuliwa changamoto zinazowakabili hata ikibidi kufika Dodoma wasisite kwenda.