Wadau wa Bajeti wameeleza kuwa suala la kuanzishwa kwa tozo katika laini za simu na tozo za miamala ni kutoza ushuru mara mbili kwa kile alichoeleza kuwa tayari serikali inatoza kodi katika maeneo hayo.
Hayo yamebainishwa katika mdahalo wa wahariri wa vyombo vya habari kujadili mapendekezo ya Bajeti kuu ya mwaka 2021/22 zikiwa zimebaki siku takribani 10 kabla ya kuanza kutumika kwa bajeti hiyo endapo itapitishwa na bunge.
Bajeti mpya ya Serikali inakusudia kutoza sh 10 hadi sh 200 kwa kila anayeongeza muda wa maongezi kulingana na matumizi ya mhusika lakini pia sh10 hadi sh 10,000 itatozwa kwenye miamala ya fedha kulingana na kiwango cha thamani ya muamala.
Mwanzilishi wa Lets Talk Finance, Edmund Munyagi, akizungumzia katika eneo hilo katika mdahalo ulioandaliwa na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) amesema kuwa tozo hiyo inaweza kuathiri ukuaji wa uchumi Dijitali.
Aidha amesema tayari serikali inatoza kodi ya ongezeko la thamani na kodi ya bidhaa kupitia vocha na makato ya kufanya miamala, hivyo tozo hiyo inayopendekezwa itaongeza gharama za uendeshaji wa simu na kupunguza matumizi wakati serikaili ilipasa kuwekeza kuvutia watu kutumia zaidi simu ili ikusanye zaidi.
Naye mtaalamu wa Uchumi Lawrance Mlaki amesema kuwa bajeti hiyo iliyosomwa siku kadhaa zilizopita inamgusa kila mwananchi na katika kila ongezeko la kodi serikali imeeleza madhumuni yake.
Aidha amesema, matumizi ya serikali ambayo imekusudia kuyafanya kupitia tozo za kodi mpya yatachochea ukuaji wa uchumi kwa kuboresha huduma za kijamii ikiwemo Afya, Miundombinu ya barabara na Elimu.
Kwa upande wake Makuamu Mwenyekiti wa TEF, Bakari Machumu, amesema lengo la mdahalo huo ni kuangalia namna ambavyo vyombo bya habari vinakuwa sehemu ya amendeleo ya Taifa kwa kuibua mijadala yenye tija kwa jamii.