Wakati Young Africans ikiondoka leo Jumanne (Februari 07) kuelekea nchini Tunisia kwa ajili ya mchezo wa kwanza wa Kundi D Kombe la Shirikisho Barani Afrika, Uongozi wa Klabu hiyo umejiongeza kwa kuutazama mchezo wa pili wa Kundi hilo dhidi ya TP Mazembe.
Young Africans itacheza dhidi ya US Monastir mwishoni mwa juma hili (Jumapili Februari 12), kisha itarejea nyumbani Dar es salaam kupapatuana na Miamba ya DR Congo TP Mazembe (Jumapili Februari 19), katika Uwanja wa Benjamini Mkapa.
Afisa habari wa Young Africans Ally Kamwe ameweka wazi mipango na mikakati ya kuelekea mchezo huo wa pili wa Kundi D, alipozungumza na Waandishi wa Habari mapema leo Jumanne (Februari 07).
Kamwe amesema wanafahamu umuhimu wa mchezo huo kwa kuhakikisha wanapata ushindi, kutokana na dhamira waliojiwekea na kushinda michezo yote ya nyumbani ya Kimataifa.
Amesema kutokana na suala hilo, Uongozi wa Young Africans umeona kuna umuhimu wa kuupa jina maalum mchezo huo na kuuita WANANCHI SUPER SUNDAY, kwa maana ndio utakuwa mchezo mkuwa barani Afrika kwa hiyo siku ya Jumapili.
Amesema Tiketi za mchezo huo zitaanza kuuzwa mapema, ili kutoa nafasi kwa Mashabiki na Wanachama wengi wa Young Africans, kujiandaa na siku hiyo muhimu, ambayo itawalazimu kupata alama tatu za nyumbani, baada ya kucheza ugenini dhidi ya US Monastir.
“Hii siku ya Jumapili dhidi ya TP Mazembe ni muhimu sana, na tumeipa jina maalum, WANANCHI SUPER SUNDAY, maana ndio utakuwa mchezo mkuwa barani Afrika kwa hiyo siku ya Jumapili”
“Tunajua umuhimu wa kushinda mechi za nyumbani, hivyo tunahitaji sana uwepo wa mashabiki kuwapa nguvu na kuwapa hamasa wachezaji wetu na ndio maana tunaanza kuuza tiketi mapema ili kila mtu apate fursa ya kushiriki kwenye hii WANANCHI SUPER SUNDAY” amesema Afisa habari Young Africans Ally Kamwe.