Kikosi cha Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans kitaondoka jijini Dar es salaam leo Jumanne (Februari 07) kuelekea Tunisia, tayari kwa mchezo wa Kwanza wa Kundi D, Kombe la Shirikisho Barani Afrika.

Young Africans itacheza ugenini Jumapili (Februari 12) dhidi ya US Monastir katika Uwanja wa Hammadi Agrebi, Tunis, mishale ya saa Kumi na Moja kwa majira ya Tunisia.

Afisa Habari wa Klabu hiyo Kongwe katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati Ally Kamwe amesema, wachezaji 25, Maafisa wa Benchi la Ufundi na baadhi ya Viongozi wataanza safari jijini Dar es salaam majira ya saa tisa alasiri.

Kamwe amesema katika msafara huo, atakuwepo Mlinda Lango Aboutwalib Mshery, ambaye anakwenda Tunisia kwa sababu maalum za kupatiwa matibabu, kufuatia jeraha lake la Goti ambalo limemuweka nje kwa majuma kadhaa.

“Tunaondoka Dar es Salaam leo saa 9:25 alasiri kuelekea Dubai, ambapo tutapumzika hapo na kesho tutaondoka kuelekea Tunisia, tunasafiri na wachezaji 25 na benchi la ufundi 6 pamoja na Aboutwalib Mshery akienda kwa ajili ya matibabu na Mwalimu Nabi akiwa ameshatangulia Tunisia kwa ajili ya maandalizi” Afisa habari Young Africans Ally Kamwe.

Baada ya mchezo dhidi ya US Monastir, Young Africans itarejea nyumbani Dar es salaam kucheza dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo Februari 19, kisha itakwenda nchini Mali kuikabili Real Bamako, katika Uwanja wa du 26 Mars, mjini Bamako Februari 26.

Machi 08, Young Africans itacheza Mchezo wa Mzunguuko wa Nne wa Kundi D dhidi ya Real Bamako Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, Kabla ya kuikaribisha US Monastir Machi 19. Wananchi watamalizia ugenini kwa kukabili TP Mazembe mjini Lubumbashi katika Uwanja wa TP Mazembe, April 02.

Rais US Monastir aichambua Young Africans
Carlos Queiroz abeba jukumu zito Qatar