Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania – TPA, Plasduce Mbossa ametolea ufafanuzi juu ya azimio la Serikali kuingia katika ushirikianno wa kiuchumi na kijamii na Serikali ya Dubai kwa ajili ya uendelezaji, uboreshaji na utendaji wa kazi za Bandari nchini.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa hii leo Juni 7, 2023 na TPA imeeleza kuwa Juni 5, 2023, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilitoa Taarifa kwa Umma kuhusu mwaliko wa Wadau wote kutoa maoni kuhusu Azimio la Bunge la mapendekezo ya Kuridhia Makubaliano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Dubai kuhusu ushirikiano wa Kiuchumi na kijamii kwa ajili ya Uendelezaji na Uboreshaji wa Utendaji kazi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania la Mwaka 2023.
Imesema, “kufuatia Taarifa hiyo kwa Umma iliyotolewa kupitia tovuti ya Bunge, kumekuwa na upotoshaji katika mitandao ya kijamii kwamba “Serikali imepanga kuipa kampuni ya DP World ya Falme ya Dubai kandarasi ya uendeshaji wa shughuli za Bandari ya Dar es Salaam kwa muda wa miaka mia moja (100)”.
Aidha, imefafanua kuwa, “kufuatia kusambaa kwa taarifa hizo, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) inapenda kuwajulisha Wateja, Wadau wa Kitaifa na Kimataifa na Umma kwa ujumla kwamba, taarifa hizo sio sahli, ni upotoshaji unaofanywa kwa makusudi na watu wenye nia ovu ya kukwamisha mipango thabiti ya Nchi katika kuongeza ufanisi wa Sekta ya Bandari Nchini kwa maslahi mapana ya Taifa.”
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, “Taarifa sahihi ni kuwa, Azimio la Bunge linahusu Mkataba ambao Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaingia na Serikali ya Dubai wenye ukomo wa miezi kumi na mbili (12) kwa ajili ya kutoa nafasi kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kujadiliana na Serikali ya Dubai kuhusu maeneo ambayo Serikali hizo mbili zinaweza kushirikiana katika uboreshaji na uendelezaji wa Sekta ya Bandari Nchini Tanzania.”
Taarifa hiyo imesema, “Ushirikiano wa Nchi mbili za Dubai na Tanzania una lengo la kuongeza ufanisi wa huduma za Bandari Nchini, kukuza ajira za Watanzania na kufungua fursa za kiuchumi na kijamii kupitia uwekezaji kwenye baadhi ya maeneo ya Bandari ya Dar es Salaam, maeneo huru ya kiuchumi na viwanda (Special Economic and Industrial Zones) kwa kujenga viwanda pamoja na uwekezaji katika mnyororo mzima wa usafirishaji kutoka Bandari za Tanzania kwenda Nchi za jirani ambazo zinatumia Bandari zetu.”
Aidha, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) inawaomba Wateja, Wadau na Umma kutambua kwamba, jitihada zote na hatua zinazochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Sita katika kuvutia uwekezaji Nchini hususan kwenye maeneo ya Banadari, zinalenga kumaliza changamoto za muda mrefu ikiwemo ucheleweshwaji wa meli, mizigo na kukosekana kwa ufanisi katika Bandari zetu.