Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC), imetoa siku saba kwa bondia Hassan Mwakinyona Kampuni ya Paf Boxing, kutoa sababu za kutofanyika kwa pambano kati ya Mtanzania huyo na Julius Indongo kutoka Namibia.
Ijumaa (Septemba 29), Mwakinyo alipaswa kuvaana na Indongo katika pambano la mkanda wa Ubingwa wa Mabara (IBA) uzito wa kati, lakini pambano la mabondia hao halikufanyika huku sababu sahihi zikiwa hazijawekwa wazi.
Pamoja na Mwakinyo na Indongo kutopigana, lakini mabondia wengine waliopangwa kucheza mapambano ya utangulizi katika Ukumbi wa Ubungo Plaza, Dar es salaam, walivaana.
Akizungumza Dar es Salaam, Katibu wa TPBRC, George Lukindo alisema kamisheni imetoa siku saba kwa promota wa pambano hilo, Godson Karigo na Mwakinyo, kutoa sababu za kushindwa kufanyika kwa pambano hilo.
“Ndani ya siku hizi saba tunahitaji kupata maelezo kutoka kwa wahusika wote wawili yaani promota na Mwakinyo, kipi kimesababisha hadi akashindwa kucheza,” alisema Lukindo.
Katibu huyo alisema tukio hili, linaweza kusababisha kushuka kwa heshima ya mchezo wa masumbwi nchini.
Tunaomba radhi kwa tukio lililotokea kwa sababu mchezo huu sasa hivi umekuwa na mashabiki wengi, hivyo hatuhitaji kuona tunapoteza hamasa ambayo imetengenezwa kwa juhudi kubwa,” alisema.