Saa 24 baada ya Mabingwa wa Kombe La Shirikisho Tanzania Bara (ASFC) Azam FC kuwasilisha barua ya malalamiko dhidi ya waamuzi watatu waliosimamia mchezo wao dhidi ya Young Africans, Afisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TPLB) Almas Kasongo amesema wamepokea barua hiyo.
Waamuzi watatu waliolalamikiwa na Azam FC ni Heri Sasii aliyekuwa mwamuzi wa kati na wasaidizi wake Soud Lila na Mbaraka Haule, ambao walipewa jukumu la kuhakikisha wansimamisha vyema sheria 17 za mchezo wa soka kati ya mabingwa watetezi wa ASFC dhidi ya Young Africans, Jumapili (Juni 21) Uwanja wa taifa Dar es salaam.
Kasongo amesema kuwa wamepokea barua kutoka uongozi wa Azam FC leo (Jumanne) wataijadili pamoja na kujadili matukio mengine ambayo yametokea kwenye Ligi Kuu Bara na Ligi Daraja la Kwanza.
“Tumepokea barua kutoka Azam FC ambayo inaeleza kuhusu mechi yao ya iliyochezwa dhidi ya Yanga, Uwanja wa Taifa, leo kamati itakutana ili kujadili kwani kazi yetu ni kufanyia kazi matukio ambayo yanatokea na kutoa adhabu kwa mujibu wa kanuni,” amesema.
Katika barua hiyo waliyoiwasilisha Bodi Ya Ligi, Azam FC imeyalalamikia maamuzi matatu waliyodai yana utata ambapo dakika ya kwanza bao la beki Abdallah Kheri akifunga kwa kichwa akitumia krosi ya Iddi Seleman lilikataliwa kwa madai mfungaji alikuwa katika eneo la kuotea jambo ambalo halikuwa la kweli.
Tukio lingine ni lile la dakika 47 ambapo mshambuliaji Never Tigere bao lake lilikataliwa akidaiwa ameotea wakati akipokea pasi ya Richard Djodi ingawa picha za marudio ya luninga zilionyesha kuwa hakuotea.
Tukio la tatu ambalo Azam wamelijumuisha katika malalamiko yao ni lile la dakika 75 ambapo beki wao wa kulia Nicholas Wadada aliangushwa ndani ya eneo la hatari wakidai lilipaswa kutafsiriwa kuwa penalti lakini haikuwa hivyo.
Aidha Azam imesema inatarajia matukio hayo yatafanyiwa uchunguzi na bodi hiyo huku wakiambatanisha malalamiko yao sambamba na vipande vya video vya matukio hayo.
Wameongeza kwamba matukio hayo yamekuwa yakijirudia kwa timu yao kutotendewa haki ambapowana amini haki itatendeka kwa mujibu wa sheria na kanuni.