Bodi ya Ligi Tanzania Bara ‘TPLB’ imetoa ratiba ya michezo ya Mtoano (Play Off) kwa timu za Ligi Kuu Tanzania Bara Mtibwa Sugar na Tanzania Prisons, ambazo zimemaliza katika nafasi ya 13 na 14.
Kikanunia timu hizo zinapaswa kucheza ili kupata timu itakayobaki Ligi Kuu na nyingine itakayocheza na timu moja kutoka Ligi Daraja la Kwanza (JKT Tanzania), inawania kupanda Ligi Kuu msimu wa 2022/23.
Taarifa ya TPLB imeeleza kuwa, mchezo wa mkondo wa kwanza umepangwa kuchezwa kweshokutwa Jumapili (Julai 03), katika Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, ambapo Tanzania Prisons itakua mwenyeji wa Mtibwa Sugar.
Mchezo wa Mkondo wa pili utachezwa siku tatu baadae (Julao 06), katika Uwanja wa Manungu Complex mkoani Morogoro, ambapo Mtibwa Sugar itakua mwenyeji wa Tanzania Prisons.
Atakayepoteza michezo hiyo kwa matokeo ya jumla atacheza na JKT Tanzania ambayo itaanzia nyumbani Julai 09, kisha itamalizia ugenini kwa mchezo wa mkondo wa pili uliopangwa kupigwa Julai 13. Mshindi wa jumla katika michezo hiyo atacheza Ligi Kuu Tanzania Bara, atakayepoteza atacheza Ligi Daraja la Kwanza msimu wa 2022/23.