Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imewahimiza wamiliki wa majengo yaliyopimwa na ambayo hayajapimwa kulipia kodi stahiki za majengo wakiwemo wote wenye madeni kufanya hivyo ili kuepuka usumbufu wa kimfumo pindi wanapolipa kwa pamoja.
Mkurugenzi wa kitengo cha elimu kwa mlipa Kodi Richard Kayombo, amesema kufanya hivyo ni sehemu ya wananchi kutimiza wajibu hasa katika robo hii ya kwanza.
“Kwa kawaida wamiliki wote wa majengo yanatakiwa kulipiwa kodi ikiwa imepimwa au haijapimwa na ni vyema wananchi wafanye hivyo kwa maana zile siku za mwisho huwa zina changamoto kubwa zinazopelekea mifumo kuzidiwa.”amesema Kayombo.
Amesema, mamlaka hiyo inaendelea na mpango wake wa kutembelea mlango kwa mlango kutoa elimu ya kodi lakini pia kuzifahamu changamoto za wafanyabiashara moja kwa moja.
“Hili zoezi tayari tunaanza kulitekeleza kwa mikoa ya Arusha,Mtwara,Kagera,Tabora, na Dar es salaam tufanya katika Wilaya ya Ubungo lengo ikiwa tunataka kila mwananchi apate uelewa kuhusu masuala ya kodi.” amesema Kayombo.
Kayombo, amewataka waajiriwa kuhakikisha wanakabidhi utambulisho wa mlipa kodi (TIN), kwa waajiri wao zoezi ambalo limeongezwa muda hadi mwezi disemba 2020, ambapo wahusika watafanya maombi haya kwa njia ya kimtandao.