Kamishna Mkuu, wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Alphayo Kidata, amesema mamlaka hiyo imekusanya imekusanya Sh12.4 trilioni katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha 2022/23 yaani Julai hadi Desemba 2022, Makusanyo hayo ni sawa na asilimia 99 ya lengo la makusanyo ya Sh12.48 trilioni.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TRA na kusainiwa na Kamishna Mkuu Kidata, imesema makusanyo hayo ni sawa na ongezeko la Sh1.35 trilioni ikilinganishwa na Sh11.11 trilioni iliyokusanywa kipindi kama hicho Mwaka wa Fedha 2021/22.
“Ongezeko hili ni sawa na ukuaji wa makusanyo wa asilimia 12.2,” imeeleza taarifa hiyo hatahivyo, katika kipindi cha Desemba 2022, TRA imefanikiwa kukusanya Sh2.77 trilioni kati ya lengo la kukusanya Sh2.60 trilioni.
Makusanyo hayo ya Desemba 2022 yanatajwa kuwa na ufanisi wa asilimia 106.5, sawa na ukuaji wa asilimia 10.3 ukilinganisha na makusanyo ya Desemba 2021
Tunaendelea kuwashukuru walipakodi nia wadau wetu mbalimbali kwa kujitoa kwenu katika kipindi cha nusu mwaka ambapo mwenendo wa ulipaji kodi kwa hiari na uhusiano baina ya mamlaka na walipakodi umeendelea kuimarika kwa kiwango cha kuridhisha.
TRA imesema inaendelea kufanyia kazi malekezo na miongozo ya Serikali juu ya namna bora ya kukusanya mapato bila matumizi ya nguvu na hivyo kuendelea kujenga mazingira wezeshi ya uwekezaji ya ufanyaji biashara nchini.
Vilevile, TRA inaeleza kwamba itaendelea kuboresha huduma kwa Walipakodi kwa kuzingatia dhana ya uadilifu, weledi na uwajibikaji ili kujenga taswira yenye kuaminika katika jamii
“Pamoja na mafanikio tuliyoyapata, bado upo umuhimu wa kuongeza kiwango cha makusanyo kwa kuinua kiwango cha ulipaji kodi kwa hiari kwa walipakodi ili kuiwezesha Serikali kuongeza wigo wa utoaji huduma kwa wananchi wote kama vile ulinzi, miundombinu ya barabara, huduma za kijamii zikiwemo elimu, afya, maji, umeme,” amesema Kidata katika taarifa yake.