Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imesema ifikapo Januari 31, 2021 wafanyabiashara wasiotumia mfumo wa Stempu za Kodi za Kielektroniki (ETS) ulioanza kutumika Novemba 1, mwaka huu hawataruhusiwa kuingiza bidhaa zao sokoni.
Taarifa iliyotolewa leo Desemba 30 na TRA imezitaja bidhaa hizo kuwa pamoja na juisi za matunda na mbogamboga, maji ya kunywa yaliyofungashwa kwenye chupa, na bidhaa za fllamu na muziki (yaani,CD/DVD/Kanda zilizorekodiwa).
“Hatua hii inafuatia kukamilika na kuanza kwa matumizi ya mfumo huu kwa awamu ya kwanza na awamu ya pili kwa bidhaa za sigara, mvinyo, pombe kali, bia, na aina zote za vileo tangu Januari 15, 2019 na kwa bidhaa za vinywaji laini mnamo tangu Agosti 1, 2019 mtawalia,” imesema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo imerejea kifungu cha 5(1)(a) cha Sheria ya Mamlaka ya Mapato Tanzania, sura ya 399 R.E 2019 ikitahadharisha uzalishaji na uingizaji wa bidhaa hizo sokoni bila stempu hizo.
TRA imesema kwa kuwa bidhaa hizo hazikuwa zikibandikwa stempu hapo awali, hivyo basi, bidhaa zote zilizopo sokoni na kwenye maghala ya watengenezaji au waingizaji wa bidhaa hizo, ambazo hazijabandikwa stempu hizo zinaruhusiwa kuendelea kuuzwa kwa kipindi kisichozidi miezi mitatu (3), yaani, ama kabla au hadi kufikia Januari 31, 2021.
Wazalishaji na waagizaji wametakiwa kutoa taarifa kwa TRA juu ya idadi ya bidhaa walizonazo ambazo hazijabandikwa stempu za kodi za kielektroniki kabla ya tarehe rasmi ya kuanza matumizl ya mfumo huu kwa kujaza fomu maalum inayopatikana kwenye ofisi za TRA za kila Mkoa na katika tovuti ya Mamlaka hiyo (www.tra.go.tz).
Baada ya Januari 31, 2021, bidhaa zote ambazo hazijawekewa stempu za kielektroniki hazitaruhuslwa kuwepo sokoni mpaka zitakapobandikwa Stempu za Kodi za Kielekroniki.