Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un ameanza safari yake kwa Treni kuelekea nchini Vietnam ambapo atakutana kwa mara ya pili na Rais wa Marekani, Donald Trump.
Kim alianza safari yake Jumamosi jijini Pyongyang, akiwa ndani ya treni yenye silaha nzito na kusindikizwa na ulinzi mkali ambapo alipita katika ardhi ya China.
Treni hiyo ilionekana ikivuka daraja jijini Beijing na inaelezwa kuwa leo itakuwa ikipitia Magharibi kuelekea Vietnam. Vyanzo vya kuaminika vimeliambia Shirika la Habari la AFP kuwa Kim Jong Un atafika kwenye kituo cha treni cha Dong Dang, kilichoko mpakani Jumanne wiki hii.
Ulinzi mkali umeshuhudiwa katika kituo hicho cha treni cha Dong Dang kuanzia mapema leo asubuhi, kituo hicho kinalindwa na vikosi vya jeshi huku kikiwa kimefungwa kuzuia matumizi ya umma ya kawaida.
“kituo cha treni kimefungwa, hakuna raia yeyote anayeonekana hapa. Hatujui kitafungwa hadi lini, lakini inawezekana ikawa hadi kesho usiku,” mwandishi wa AFP amemkariri mlinzi wa eneo hilo ambaye hakutaka kufahamika.
Kim Jong Un atawasili katika kituo hicho Jumanne jioni baada ya safari a Kilometa 4,000 akitumia siku mbili na nusu.
Msafara wa magari yatakayompokea katika kituo cha Dong Dang utaelekea Hanoi kwa mwendo na njia ambazo bado hazijafahamika kwa umma, na safari yake ya Kilometa 170 kwa gari itakamilika kati ya saa 12 jioni na saa mbili usiku wa kesho.
Trump na Kim watakutana Februari 27 hadi 28, Hanoi nchini Vietnam kwa ajili ya mazungumzo kuhusu makubaliano ya silaha za nyuklia pamoja na mambo mengine ya kiusalama na uchumi kati ya nchi zao ambazo zilikuwa na uhasama kwa miongo kadhaa.