Rais wa Marekani Donald Trump ameihakikishia nchi yake kuwa wakati wa utawala wake ataidhibiti Iran isiendelee na mpango wake wa nyuklia, akiitaja kuwa nchi inayofadhili ugaidi.
Akilihutubia taifa hilo jana, ikiwa ni siku moja tangu Iran ishambulie kambi mbili za jeshi la Marekani zilizoko nchini Iraq kama hatua ya kulipa kisasi cha kuuawa kwa kamanda wao, Qassem Soleimani, Trump amemuelezea kamanda huyo kama ‘gaidi hatari zaidi duniani’.
“Kama Mkuu wa Jeshi la Quds, Soleimani alihusika katika mashambulizi mengi, mikono yake ilikuwa imejaa damu za Wamarekani na Wairan na alitakiwa kuwa ameuawa siku nyingi zilizopita,” alisema Rais Trump.
“Kumuua Soleimani kumetuma ujumbe kwa magaidi wote duniani kuwa kama unathamini maisha yako mwenyewe hautatishia maisha ya watu wetu,” aliongeza.
Trump alisema kuwa Kamanda Soleimani alikuwa amepanga kufanya mashambulizi megine dhidi ya Wamarekani.
Katika hatua nyingine, Trump alisema kuwa mashambulizi ya kulipiza kisasi yaliyofanywa na majeshi la Iran kwenye kambi za kijeshi za Marekani hayakuwa na madhara yoyote.
Alidai hakuna mtu aliyefariki na hakukuwa na aliyepata majeraha makubwa. Kwa mujibu wa wake, Jeshi la Marekani lilipata taarifa mapema kuhusu kufanyika kwa mashambulizi hayo na likachukua tahadhari zote.
Lakini taarifa hiyo ya Rais Trump inakinzana na taarifa iliyotolewa na Iran, ambao wameeleza kuwa mashambulizi hayo yamesababisha vifo vya ‘magaidi 80 wa Marekani’.
Iran imeapa kuendelea kulipa kisasi dhidi ya hatua za Marekani. Kifo cha Kamanda Soleimani ambaye anaheshima kubwa nchini Iran kama mwanamapinduzi na shujaa kimeamsha hasira za nchi hiyo, akizikwa na maelfu.
Iran, imetangaza rasmi kuvunja mkataba wa mpango wa nyuklia kati yake ya Marekani, na inaendelea na uzalishaji kama kawaida.
Rais Trump alidai kuwa ili kuidhibiti Iran isiendelee na mpango wake wa Nyuklia, wataweka vikwazo vipya vya kiuchumi dhidi ya nchi hiyo; na kwamba Marekani inaweza kuishi bila kutegemea mafuta kutoka Mashariki ya Kati.