Rais wa Marekani, Donald Trump amemshukuru Rais wa Urusi Vladimir Putin kwa kuwafukuza wafanyakazi 755 kutoka nchini humo na wale waliokuwa wakifanya kazi katika ubalozi wa Marekani nchini humo.
Trump amesema kuwa anamshukuru sana Putin kuwafukuza Wamarekani hao kwani ameipunguzia gharama kubwa Marekani iliyokuwa ikitumia kuwalipa wafanyakazi hao.
Aidha, pamoja na Trump kusema hayo lakini bado uchunguzi unafanyika nchini Marekani kubaini kama kulikuwa na ushirikiano kati ya maafisa wa kampeni wa Trump na Urusi, kuingilia uchaguzi mkuu wa mwaka 2016.
Mwishoni mwa mwezi Julai, Rais Putin alitangaza kuwafukuza wafanyakazi 755 Wamarekani kuondoka kutoka ofisi za kibalozi za Marekani nchini Urusi, huku akilipiza kisasi cha hatua ya Marekani kuiwekea vikwazo Moscow.
“Ningependa kumshukuru kwa sababu tunajaribu kupunguza wafanyakazi wetu na kwangu mimi namshukuru sana kwamba amewafukuza watu wengi kiasi hicho,” amesema Trump.
Hata hivyo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imesema kuwa hatua hiyo iliyochukuliwa na Rusia inasikitisha kwakuwa inazorotesha mahusiano kati ya nchi hizo.