Rais wa Marekani, Donald Trump amesema kuwa hataweka sheria ya kuwalazimisha watu kuvaa barakoa ingawa visa vya corona vinazidi kuongezeka nchini humo.
Hadi leo, Marekani imeshathibitisha visa vya corona milioni 3.68, vifo zaidi ya 141,000 na watu zaidi ya milioni 1 wamepona.
Akizungumza kwenye mahojiano na Fox News, Trump amesema kuwa angependa kuona watu wanakuwa huru na kufanya uamuzi kwa utashi wao zaidi.
Ameongeza kuwa ingawa anaamini barakoa ni nzuri na ni sehemu ya jitihada za kupambana na maambukizi ya virusi vya corona, anafahamu huleta madhara pia.
“Hapana, nataka watu wawe na uhuru kiasi fulani na siamini katika kuwalazimisha kuvaa barakoa. Hapana, na sikubaliani na matamko kuwa kama kila mmoja atavaa barakoa basi ghafla virusi vitatokomea,” alisema Rais Trump.
“Kila mtu alikuwa anasema tusivae barakoa na ghafla kila mtu akawa anavaa barakoa, na kama unavyojua, barakoa husababisha matatizo pia. Pamoja na yote yanayosemwa, mimi ni muumini wa barakoa, ninadhani barakoa ni nzuri,” aliongeza.
Wakati Trump akiweka msimamo wa kutotunga sheria ya barakoa, Serikali ya Uingereza imetunga sheria inayowabana watu wasiovaa barakoa wanapoenda kufanya manunuzi kwenye maduka mbalimbali, kwa kuwapiga faini ya £100 (Sawa na Sh. 263,000 za Tanzania).
Kiwango hicho cha faini kwa mtu aliyekaidi amri hiyo kinapaswa kulipwa moja kwa moja kwa polisi.