Rais wa Marekani Donald Trump ameusaini muswada wa sheria wa dola Bilioni 900, unaokusudia kutoa misaada kwa watu walioathiriwa na janga la virusi vya Corona ambao kwa siku kadhaa tangu ulipopitishwa wiki iliyopita na Bunge, alikataa kuusaini akiutaja kuwa fedheha..
Kulikuwa na wasiwasi kwamba kuchelewa kufanya hivyo, kungesababisha baadhi ya faida za ukosefu wa ajira kupotea, ikimaanisha kwamba mamilioni ya watu wangeweza kupoteza pesa wakati huu mgumu wa uchumi uliochangiwa na janga la virusi vya corona.
Mpango huo unaotoa misaada ya dharura ya janga la virusi vya Corona, ni sehemu ya muswada mkubwa wa matumizi ambao pamoja na saini ya Trump, utasaidia kuepusha shughuli za serikali kufungwa.
“Ninasaini muswada huu kurejesha manufaa ya ukosefu wa ajira, kuzuia watu kuondolewa kwenye nyumba, kutoa misaada, kuongeza pesa katika programu za ulinzi wa malipo, kurudisha wafanyakazi wetu wa ndege kazini, kuongeza pesa zaidi katika usambazaji wa chanjo na mengi zaidi”, amesema Trump.
Hatua ya Trump kubadili msimamo imekuja baada ya simu kutoka pande zote za kisiasa za kumtaka achukue hatua za kuepusha maafa ya kiuchumi na kijamii, hasa kwa wamarekani wengi walio katika mazingira magumu.
Trump amesisitiza kwamba malipo ya moja kwa moja yaongezwe kutoka dola 600 katika muswada hadi dola 2000.