Rais wa Marekani, Donald Trump amezungumzia maendeleo ya uhusiano kati yake na Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un na kueleza kuwa watakutana tena Februari mwaka huu.
Kupitia hotuba yake leo, Rais Trump amesema kuwa uhusiano kati ya Marekani na Korea Kaskazini umeimarika hasa kwa kuzingatia kuwa hakuna majaribio yoyote ya silaha za kinyuklia yaliyofanyika katika kipindi cha miezi 15 iliyopita.
“Tumeendelea na mpango wa kusukuma gurudumu la kutafuta amani katika eneo la Rasi ya Korea. Majaribio ya makombora ya nyuklia yamesitishwa na hakuna tena uzinduzi wa vinu vya makombora ya kinyuklia,” alisema Trump.
“Kama nisingechaguliwa kuwa Rais wa Marekani, wakati huu kwa mtazamo wangu tungekuwa kwenye vita kubwa na Korea Kaskazini. Uhusiano kati yangu na Kim Jong Un ni mzuri,” aliongeza.
Rais Trump alisema kuwa mkutano wa pili kati ya viongozi hao wawili utafanyika nchini Vietnam. Ingawa hakutaja mji husika, Hanoi na Da Nang ndio majiji yanayopewa nafasi zaidi ya kupata ugeni huo wa kihistoria.
Kim Jong Un na Trump walikutana kwa mara ya kwanza mwaka jana nchini Singapole ambapo walikubaliana kuchukua hatua za kuondoa silaha za nyuklia katika eneo la Rasi ya Korea.