Mahasimu wakubwa kwenye uchaguzi mkuu wa mwezi Novemba nchini Marekani, Donald Trump kutoka chama cha Republican na Joe Biden wa Democratic, wametumia mdahalo wao wa kwanza kushambuliana jinsi familia zao zilivyofaidika na kuwapo kwao madarakani.
Wakati Biden alipokuwa akizungumzia jinsi mikataba ya kibiashara ya Marekani na China isivyoleta tija iliyokusudiwa, Trump alimkatiza akitaja kuhusika kwa mtoto wa Biden, Hunter Biden, kwenye biashara nje ya nchi, hasa Ukraine.
Kwa upande wake, Biden ambaye ni mgombea kutoka chama cha rais aliyepita wa Marekani, Barack Obama, amesema ingechukua usiku mzima kuzungumzia familia ya Trump ambaye anawania muhula wake wa pili, laiti angelitaka hilo.
Mbali ya mikataba ya kibiashara, mdahalo huo uliofanyika usiku wa kuamkia leo, ulitandwa pia na shutuma na tuhuma baina yao kuhusiana na masuala kadhaa, yakiwemo janga la virusi vya corona, mfumo wa afya, uchumi, usalama na ubaguzi wa rangi, na athari za mabadiliko ya tabia nchi, ambapo Biden aliahidi kuirejesha Marekani kwenye mkataba wa Paris, ambao unalenga kupunguza uzalishaji wa gesi chafu.