Mwenyekiti mpya wa Bodi ya Wakurugenzi ya Klabu ya Simba Salim Abdallah ‘Try Again’ ameridhia baada ya Mohamed Dewji ‘Mo’ kumkasimisha madaraka hayo.
Mapema leo Jumatano (Septemba 29) majira ya asubuhi Mo kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii alithibitisha kuachia nafasi hiyo na kumkabidhi aliyekuwa Makamu wake Try Again akiamini anaweza kutokana na ukongwe wake katika soka.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa jukumu la mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Simba SC Try Again amesema, amepokea nafasi hiyo bila kinyongo na ataifanyia kazi vilivyo licha ya kuwa ngumu.
“Ni kweli Mohamed ameachia hiyo nafasi, na mimi ndiye nitachukua nafasi yake, nimeipokea kwa mikono miwili naamini kwa kushirikiana na wenzangu tutafikia malengo yetu,”amesema.
Maamuzi ya Mo kujiondoa katika nafasi hiyo yalifanyika Septemba 21 mwaka huu katika kikao cha bodi ya wakurugenzi kilichoketi Dar es Salaam.