Mabosi wa Simba SC wameweka wazi kuwa maboresho yatakayofanywa kwenye kikosi hicho kwa msimu wa 2023/24 ni makubwa yenye malengo ya kuimarisha kikosi kitakachokuwa na uwezo wa kutwaa mataji.
Timu hiyo chini ya Kocha Mkuu, Roberto Oliveira, Raia wa Brazil imegotea nafasi ya pili kwenye ligi huku ikishuhudia Young Africans wakitwaa ubingwa wa ligi kwa mara ya pili mfululizo.
Katika anga za kimataifa imegotea Robo Fainali Ligi ya Mabingwa Afrika huku watani zao wa jadi Young Africans kwenye Kombe la Shirikisho Barani Afrika wakiwa washindi wa pili baada ya kucheza Fainali.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Salim Abdallah ‘Try Again’ amesema kuwa kwa makosa ambayo wamepitia msimu wa 2022/23 ni somo kwao.
“Makosa ambayo yametokea kwa msimu ambao umeisha ni somo kwetu na tumeona pale ambapo tulikwama kufanikiwa hasa kwa wachezaji ambao tulikuwa nao pamoja na wale ambao tuliwaacha.
“Kikubwa kwa wakati ujao ni kuona tunakuwa na timu bora itakayotufanikishia malengo yetu ya kutwaa mataji kwani hilo ndilo jambo ambalo tunalitarajia na tunaamini itakuwa hivyo.”
Tayari kikosi hicho kimeanza kupitisha panga kwa wachezaji wao ikiwa ni pamoja na Erasto Nyoni, Jonas Mkude, Augustine Okrah, Nelson Okwa, Beno Kakolanya na Victor Akpan.