Kufuatia tambo za vinara wa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Young Africans kwa kuanza kwa kasi msimu huu 2023/24 katika vita ya kutetea mataji waliyotwaa msimu uliopita, uongozi wa Simba SC umeweka wazi kuwa maneno na kasi hiyo haiwashtui na kuchimba mkwara mzito kuwa wao hesabu zao ni kubeba makombe yote.
Tangu kupoteza taji la Ngao ya Jamii mbele ya Simba SC katika Fainali iliyopigwa mkoani Tanga, Young Africans wamekuwa gumzo kutokana na kasi waliyonayo ambapo katika michezo mitatu mfululizo iliyopita ya mashindano yote wameibuka na ushindi mnono wa mabao matano na kuruhusu bao moja tu.
Kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa sasa Young Africans wanaongoza msimamo na alama zao sita sawa na Simba SC ambao wako katika nafasi ya tatu wakizidiwa kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Simba SC, Salim Abdallah Try Again’ amesema: “Kama kikosi tunajivunia kuanza vyema msimu huu kwa kufanikiwa kushinda taji la Ngao ya Jamii na dhamira yetu ya kuendelea kukusanya makombe inaendelea.
“Kumekuwa na kelele nyingi za mashabiki wa timu mbalimbali, lakini kwetu malengo makuu ni mataji na hesabu zetu ni kushinda makombe yote, hivyo kelele zao hazitutoi mchezoni.”