Wachezaji Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ wa Simba SC na Nahodha wa Young Africans Bakari Nondo wameachwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, kitakachoingia kambini kujiandaa na michezo ya kimataifa ya kirafiki.
Taifa Stars itacheza dhidi ya Libya, ikiwa ni maandalizi ya Michezo ya kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika ‘AFCON 2023’ ambapo Tanzania itacheza dhidi ya Uganda.
Kocha Janza anayekiongoza kikosi cha Taifa Stars kwa muda kufuatia kuondolewa kwa Kocha Kim Poulsen mwezi uliopita, amezungumza na Waandishi wa Habari leo Jumanne (Septemba 13) majira ya mchana na kutangaza kikosi chake kitakachoingia kambini mwishoni mwa juma hili.
Kocha huyo kutoka nchini Zambia ambaye pia ni Kocha wa Klabu ya Namungo FC, ametaja kikosi cha wachezaji 23, huku akimrejesha beki Abdi Banda anayecheza soka la kulipwa katika klabu ya Chipa United ya Afrika kusini.
Banda mara ya mwisho kuitwa kwenye timu ya taifa ni kipindi alichokuwa anacheza soka la kulipwa katika klabu ya Baroka ambayo baadae aliachana nayo na kurejea nchini msimu uliopita na kucheza Ligi Kuu akiwa na Mtibwa Sugar.
Ingizo la Abdi Banda kwenye kikosi kunamuondoa nahodha wa Young Africans, Bakari Mwamnyeto wakati huo huo David Luhende ameingia akichukua nafasi ya Mohamed Hussein ‘Tshabalala’.
Wachezaji wengine walioachwa kwenye kikosi hicho ni Shomari Kapombe, George Mpole, Reliants Lusajo, John Bocco, Farid Mussa, Kibu Denis na Jonas Mkude.
Na nafasi zao zimechukuliwa na Datius Peter (Kagera Sugar) Abdalah Mfuko (Kagera Sugar) Carlos Protas (Tusker Fc), David Ulomi (Moroka Swallows) na Said Hamis (Hatta Club).
Akizungumzia upande wa kuita sura mpya nyingi, Janza amesema imetokana na viwango ambavyo wamevionyesha kwenye timu zao.
“Sisi benchi letu ni kuangalia kila mchezaji ambaye anafanya vizuri na tunamuita kwa ajili ya kuipambania timu ya Taifa, milango bado ipo wazi kwa wachezaji wengine.” amesema Janza.
Upande wa kocha msaidizi, Mecky Maxime akizungumzia upande wa kukosekana mchezaji Tepsi Evance amesema , ”Sio yeye tu hata Sopu (Abdul Suleiman) tumewaweka kwenye timu chini ya miaka 23 kwa sababu wana mashindano yao.”
Stars inatarajia kuanza kuingia kambini Jumamosi na Jumatatu watafanya mazoezi mepesi kisha Jumanne wataondoka kwenda nchini Libya kucheza mechi za kirafiki mbili na timu hiyo kuanzia tarehe 20.