Siku chache baada ya kuondoka Chelsea FC, aliyekua Meneja wa Klabu hiyo ya jijini London Thomas Tuchel amefunguka kwa mara ya kwanza na kueleza alivyosikitishwa na maamuzi hayo.
Tayari Chelsea imeshamtangaza Graham Potter aliyekua anaitumikia klabu ya Brighton and Holve Albion kurithi mikoba ya Tuchel raia wa Ujerumani.
Tuchel amesema ameumizwa na kushangazwa na kitendo cha mabosi wa The Blues, kumtimua kutokana na mwenendo mbovu alioanza nao msimu huu licha ya kusajili.
Meneja huyo wa zamani wa Klabu Bingwa nchini Ufaransa Paris Saint-Germain ‘PSG’ alifutwa kazi tangu juma lililopita (Jumatano), baada ya mmiliki mpya wa klabu ya Chelsea, Todd Boehly kufanya mabadiliko katika bodi yake.
Tuchel ameandika ujumbe kupitia mtandao wa Twitter akisema “Ilikuwa ni wakati mgumu sana katika maisha yangu ya soka, sikuwahi tegemea kama nitaandika hvi, nimeumia sana maisha yangu ndani ya Chelsea yamefikia tamati, nilijikia kama nipo nyumbani, nawasukuru benchi zima la ufundi, wachezaji na mashabiki kwa kunikaribisha tangu mwanzo, najivunia niliisaidia timu kubeba ubingwa wa Ligi Mabingwa Ulaya na Kombe la Dunia kwa ngazi ya klabu, hii kumbukumbu nitabaki nayo daima”
Tuchel alizua gumzo baada ya kufukuzwa kazi Chelsea huku wadau wa soka nchini England wakihoji uwamuzi wa mabosi kwani ligi bado ilikuwa mbichi na alistahili kupewa nafasi kutokana na usajili wa wachezaji aliofanya.
Kabla kufukuzwa kazi Mjerumani huyo aliboresha kikosi chake kwa kumsajili Raheem Sterling, Kalidou Koulibaly, Pierre-Emerick Aubameyang na Wesley Fofana lakini sasa mastaa hawa watakuwa chini ya Potter aliyeteuliwa hivi karibuni.