Chama cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara, Taasisi za Fedha, Huduma na Ushauri (TUICO), leo Aprili 27, 2023, kimeendesha Warsha ya Siku Moja iliyowaleta pamoja Viongozi Waandamizi wa makampuni zaidi ya 30 kwa lengo la kuimarisha Uhusiano Bora baina ya TUICO na Taasisi za Kazi Mkoani Morogoro.
Akimkaribisha Mgeni Rasmi, ambaye alikuwa ni Kamishina wa Kazi Nchini, Mwenyekiti wa TUICO Taifa,Paul Sangeze aliwashukuru Waajiri wanaoendelea kushirikiana na TUICO katika utekelezaji wa shughuli zake ikiwa ni pamoja na kuhamasisha Wafanyakazi, uundaji wa Majukwaa na Mabaraza ya Wafanyakazi na utoaji wa Elimu kuhusu masuala mbalimbali ya kazi.
Sangeze alisema Waajiri wanatakiwa kufanya kazi na Vyama vya Wafanyakazi, sio kama maadaui, bali kama Wadau muhimu katika kukuza Tija na Ufanisi Sehemu za Kazi kwani Vyama vya Wafanyakazi huboresha mawasiliano baina ya Wafanyakazi na Menejimenti kupitia Majadiliano.
“Vyama vya Wafanyakazi sio adui wa Waajiri. Ni sauti ya pamoja ya Wafanyakazi katika kuhamasisha Uhusiano Bora na Kudai, Kulinda na Kutetea Haki, Maslahi na Heshima,”
“Tumeendelea kuunda Majukwaa na Mabaraza ya Wafanyakazi na Kamati mbalimbali kwenye Maeneo ya Kazi ambazo kwa kiasi kikubwa zimesaidia kuimarisha Utulivu sambamba na kuongeza Tija na Ufanisi kwenye Maeneo ya Kazi,” alisema Sangeze.
Akifungua Warsha hiyo, iliyofanyika mjini Morogoro, Kamishina wa Kazi Nchini, Suzan William Mkangwa alisema Warsha hiyo imekuja wakati mwafaka kwa mustakabali wa maendeleo ya taasisi za kazi, wafanyakazi na wadau hasa katika jitihada za kupunguza migogoro sambamba na ukuzaji wa tija na ufasini sehemu za kazi.
Mkangwa alisema uwepo wa uhusiano mwema baina ya vyama vya wafanyakazi na waajiri huchangia kuweka mazingira bora ya mashauriano na majadiliano hivyo kuwa na utulivu mahala pa kazi.
Aliongeza kuwa uhusiano bora husaidia katika majadiliano ya mikataba ya hali bora za kazi na kuleta mizania ya haki na wajibu kwa wadau muhimu wa sekta ya kazi na ajira nchini.
“Dhana hii inajumuisha pande mbili au tatu katika ajira ambapo lazima kuwepo na mnyororo kati ya mwajiri na mwajiriwa na kwa upana zaidi kushirikisha vyama vya wafanyakazi na waajiri. Kila mmoja anapaswa kuwajibika. Huu ni ubunifu ambao umeoneshwa na kudhihirishwa na Chama hiki [cha Wafanyakazi TUICO],” alibainisha Mkangwa.
Akitoa salamu za Waajiri Tanzania, Afisa Mtendaji Mkuu wa Chama cha Waajiri Tanzania, ATE, Suzanne Ndomba-Doran alikipongeza Chama cha Wafanyakazi TUICO kwa kuendelea kuwaleta pamoja waajiri kwani warsha kama hii husaidia kukuza tija na ufanisi sehemu za kazi.
Kwa upande wake Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania, TUCTA, Tumaini Nyamhokya alitumia Warsha hiyo kuwakumbusha waajiri kuwafahamu zaidi waajiriwa wao pamoja na kuwasaidia wanapohitaji msaada, kutunza taarifa na kujenga utaratibu wa kuwapatia mafunzo ya kazi kulingana na mabadiliko ya mifumo ya uchumi na ajira.
Naye Msajili wa Vyama vya Wafanyakazi na Waajiri Nchini,Pendo Berege alisema kuwa semina hii ni muhimu na imekuja wakati muafaka kwani itasaidia kila mmoja kujifunza na kuelewa nafasi na wajibu wake katika sehemu za kazi ili kuleta ufanisi na tija.
Warsha hiyo ni muendelezo wa jitihada za Chama cha Wafanyakazi TUICO katika kuimarisha dhana ya majadiliano ya kijamii (social dialogue) baina ya wadau muhimu wa sekta ya kazi, kuchechemua elimu na kazi za vyama vya wafanyakazi nchini na kuimarisha uhusiano bora kati ya TUICO na maeneo ya kazi yanayofanya kazi na TUICO.