Wataalam wa masuala ya Afya wameitaka Serikali kupiga marufuku kilimo cha tumbaku na matumizi ya sigara nchini Kenya wakidai inazidi kusababisha visa vya saratani, vifo vya watu wengi, kuathiri ukuaji wa ubongo wa watoto na kuathiri watu wazima.

Mwenyekiti wa Bodi ya Kudhibiti Tumbaku nchini humo, Prof. Khama Rogo ameyasema hayo katika Kongamano la Afya na Mabadiliko ya Tabianchi na kuongeza kuwap mbali na kusababisha uchafuzi wa hewa, moshi wa tumbaku pia unachangia katika mabadiliko ya tabianchi, na bidhaa zake kama vile sigara na nikotini zina athari mbaya kwa afya ya binadamu.

Mwenyekiti wa Bodi ya Kudhibiti Tumbaku nchini Kenya, Prof. Khama Rogo. Picha ya DN.

Alisema, “haijalishi ikiwa mtu ni mvutaji au la. Asiyevuta sigara akikaa karibu na mvutaji anaathirika. Madhara hayajitokezi hapo, lakini yatajitokeza zaidi ya miaka 20 baadaye ambapo mtu anapata magonjwa ya kupumua na pia saratani ya mapafu.”

Prof Rogo aliongeza kuwa, marufuku ya Sigara ni muhimu kwani yatasaidia vijana na jamii ya wanaotumia bidhaa za nikotini zinazotokana na tumbaku ikiwemo vifaa vya kuvuta mvuke kama vile sigara za kielektroniki ambazo zinaweza kuwa na nikotini na zinasababisha uraibu.

Hata hivyo, Prof Rogo alisema madhara yatokanayo na tumbaku huonekana zaidi kwa watu wazima ambao wanapata changamoto ya kupumua na saratani ya mapafu na ya mlango wa uzazi na kwamba mara kadhaa juhudi zao za kuishawishi Serikali kupiga marufuku Sigara zimeshindikana kutokana na mapato ya bidhaa hiyo.

Awali, Afisa Mkuu wa Ubora wa Hewa katika Shirika la World Resources Institute, Dkt. George Mwaniki, alisema tafiti zimeonyesha bodaboda, Bajaji na usafiri wa umma, viwanda na uchomaji taka ni vyanzo vikuu vya hewa isiyo safi inayohatarisha maisha ya wakazi wa jiji.

Wanafunzi waonywa kupokea zawadi kwa watu wasiowafahamu
Habari Kuu kwenye magazeti ya leo Septemba 1, 2023