Bondia wa ngumi za kulipwa nchini, Twaha Kassim ‘Kiduku’, ametamba hatawaangusha mashabiki wake katika pambano la kuwania ubingwa wa WBF dhidi ya Godi Apei kutoka Afrika Kusini litakalofanyika Julai 29, mwaka huu jijini Mwanza.

Kiduku amesema anaendelea vyema na mazoezi kwa ajili ya kujiimarisha kuwapa burudani na heshima wadau wa mchezo huo wa hapa Tanzania.

Amesema lengo lake ni kuona anaendelea kutangaza vizuri kipaji chake katika kila pambano atakalopanda ulingoni na kuongeza kambi yake iko mkoani Morogoro.

“Sitawaangusha mashabiki wangu, naendelea vyema na maandalizi ili nipate ushindi katika pambano hili, tuungane pamoja kwa ajili ya kuiletea heshima nchi yetu,” amesema bingwa huyo wa mkanda wa mabara wa UBO.

Naye Kocha wa Kiduku, Charles Ilanda, amesema bondia wake yupo tayari kwa ajili ya pambano hilo na amemtaka mpinzani wake kujiandaa kupokea kichapo.

“Tunatarajia atakuwa bondia mzuri kwa sababu hatujamwona akicheza, imekuwa vigumu kwetu kupata taarifa zake, lakini huwa tunafanya maandalizi kwa ajili kupambana na bondia wa aina yoyote ile,” amesema kocha huyo.

Kiduku ambaye ni mwenyeji wa Morogoro, ameshinda mapambano 22 kati ya michezo 24 aliyopanga ulingoni.

UKIMWI kumalizika 2030 - Mkurugenzi UNAIDS
Maisha hayawi marahisi kwa kuvuta bangi - Lyimo