Jukwaa la Haki za Kiuchumi na Kijamii la Tunisia, limejibu matamshi ya Rais Kais Saied akiwatuhumu wahamiaji wa Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara kwa kusababisha uhalifu huku wakiwa na tishio la idadi ya watu.
Msemaji Romdhane Ben Amor, amesema hawajaridhishwa na maneno yaliyotumika katika hotuba ya Rais Kais kwa ubaguzi wa rangi na matamshi ya chuki.
“Tunajisikia aibu kwa hotuba ya rais (Kais Saied). Tunahisi kutoridhishwa na maneno yaliyotumika katika hotuba yake ambayo yanawanyanyapaa na kuwabagua wahamiaji wa kusini mwa jangwa la Sahara”, alisema Amor.
Wiki iliyopita, mashirika 23 ya kutetea haki za binadamu yalisema serikali tayari imeanza kuwakandamiza wahamiaji kutoka Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara huku ikifumbia macho matamshi ya chuki na ya kibaguzi.
“Rais wa jamhuri lazima awajibike na taifa la Tunisia linapaswa kutekeleza ahadi zake kuhusu mikataba ya kimataifa ya haki na tunadai kukomeshwa mara moja kwa kampeni hii ya kimfumo dhidi ya wahamiaji wa Kusini mwa Jangwa la Sahara na kuachiliwa kwa wale waliowekwa kizuizini.
Aidha wameongeza kuwa, “pili, rais lazima aanzishe mchakato kamili wa kiutawala ambapo wahamiaji haramu wa kusini mwa jangwa la Sahara wanaweza kudhibiti hali zao alisema msemaji wa Jukwaa la Haki za Kiuchumi na Kijamii la Tunisia.”
Tunisia, ni kituo kikuu cha wahamiaji wa Kiafrika wanaotaka kufika Ulaya kwa kile ambacho Umoja wa Mataifa unasema ni njia mbaya zaidi ya wahamiaji duniani na kwa mujibu wa takwimu rasmi za Italia, zaidi ya wahamiaji 32,000, ikiwa ni pamoja na Watunisia 18,000, walijaribu kuvuka kutoka Tunisia kuelekea Italia mwaka jana.