Serikali nchini, imezitaka kamati za ulinzi na usalama katika Mikoa na Wilaya zote nchini pamoja na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), kuanzisha operesheni ya kuwaibaini na kuwachukulia hatua kali za kisheria waagizaji na wasambazaji wa mifuko ya plastiki iliyopigwa marufuku na Serikali.

Agizo hilo, limetolewa Jijini Mwanza na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Khamis Hamza Khamis wakati wa ziara yake ya kutembelea mradi wa dampo la kisasa lililojengwa Kata ya Buhongwa Jijini Mwanza.

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Khamis Hamza Khamis akisalimiana na Viongozi mbalimbali wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyamagana Mkoani Mwanza wakati wa ziara yake ya kukagua mradi wa dampo la kisasa lililojengwa katika Kata ya Buhongwa Wilayani Nyamagana jijini Mwanza.

Amesema, “tumeona katika dampo hili la Buhongwa limekuwa ni kituo cha mifuko ya plastiki, hii imeonesha kuwa huko mitaani kuna watu wanaojishughulisha na biashara ya uagizaji na usambazaji wa mifuko ya plastiki isiyo na ubora. Naziagiza Kamati za Ulinzi, NEMC na Mabaraza ya Halmashauri ya Wilaya kusimamia mianya yote inayopenyeza mifuko hii.”

Ameongeza kuwa, Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais ilipiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki kutokana na athari za mazingira na pia mifuko hiyo kuwa hatarishi kwa afya za wananchi, hata hivyo wapo baadhi ya watu wamekuwa wakikiuka katazo la matumizi ya mifuko hilo lililotolewa na Serikali mwaka 2019.

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Khamis Hamza Khamis akipata maelezo kuhusu mradi wa dampo la kisasa mradi wa dampo la kisasa lililojengwa katika Kata ya Buhongwa Wilayani Nyamagana jijini Mwanza kutoka kwa Meneja wa Mradi huo Desderius Polle wakati wa
ziara yake ya kukagua mradi huo.

Naibu Waziri Khamis, amefafanua kuwa nadharia za kisayansi zimedhibitisha kuwa mifuko ya plastiki inaathari kubwa kimazingira kutokana na kuchukua kipindi kirefu kutekeleza na kuoza kuanzia miaka mitatu na kuendelea na hivyo kuleta tishio kwa kubwa kwa maisha na ustawi wa viumbe na binadamu.

Katika hatua nyingine, Waziri Khamis ameipongeza Halmashauri ya Jiji la Mwanza kwa kuanzisha mradi huo ambao utasaidia juhudi za Serikali za kutotumia fedha nyingi kwenye ununuzi wa vifaa tiba kwa kuwa taka zinazozalishwa katika Jiji la Mwanza zitapelekwa kwa wakati katika dampo hilo na kunusuru magonjwa ya mlipuko.

Serikali yafurahia utekelezaji miradi ya maendeleo
GGML kinara ushiriki nyanja za kijamii