Rais wa Shirika la kutetea utawala bora na uwajibikaji – PSG, Balozi Esther Waringa ametaka kubadilishwa kwa mfumo wa uongozi na kupigwa marufuku kwa uchaguzi wa viongozi kupitia uchaguzi mkuu nchini Kenya kwani umekuwa ukileta madhara kuliko faida.
Waringa ambaye alikuwa akiwahutubia Wanahabari jijini Nairobi, alipendekeza kusimamishwa kwa Serikali ya sasa, Vyama vya upinzani, na vipengele vya Katiba ya Kenya vinavyohimiza uendeshaji wa masuala ya taifa hilo kupitia viongozi waliochaguliwa.
Amesema, “tunapigia debe kuanzishwa kwa Mfumo wa Utawala wa Huduma kwa Umma ili kuokoa nchi hii kutoka kwa uchaguzi wa kila baada ya miaka mitano ambao ni ghali na huleta migawanyiko, uharibifu na hata maafa.”
Aidha, Bi Waringa ameongeza kuwa chini ya mfumo wa Serikali ya Utumishi kwa Umma, shughuli zitaendeshwa na kusimamiwa na watumishi wa umma katika Wizara kuanzia Wakurugenzi Wakuu hadi watumishi wa Umma wa ngazi za chini.
“Maafisa hawa wataendesha shughuli za utoaji maendeleo na utoaji huduma kama vile za maji, elimu, kilimo, kawi, usalama miongoni mwa nyingine. Maafisa hawa watukuwa wameajiriwa katika wizara za serikali, lakini hawatakuwa wameteuliwa na wanasiasa,” alisema.
Bi Waringa alisema kuwa chini ya utawala anaopendekeza, maafisa watakaouendesha watakuwa ni watu ambao wameteuliwa na jopo maalum kwa kuzingatia uhitimu wao “wala sio miegemeo yao ya kisiasa.”
“Watumishi hawa wa serikali watakuwa wameteuliwa na asasi za kiusalama kama vile Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF), Makamanda wa Usalama na Maafisa wa Utawala wa Mkoa hadi ngazi za machifu na manaibu chifu,” alifafanua.
Bi Waringa, ambaye alikuwa ameandamana na wakurugenzi wa PSG Sheikh Mohamed Khan na Arvinder Sigh Mehta, alisema chaguzi kuu ambazo zimeandaliwa nchini Kenya tangu kupata uhuru kwa Taifa hilo, zimeleta madhara ya uongozi nchini kuliko faida.