Aliyekua kocha mkuu wa mabingwa wa soka Tanzania bara Wekundu Wa Msimbazi Simba Patrick Aussems (Uchebe), ameripotiwa kupoteza kibarua kwenye klabu ya Black Leopards FC ya Afrika Kusini.
Kocha huyo kutoka nchini Ubelgiji amepoteza nafasi ya ajira klabuni hapo ikiwa ni siku kadhaa baada ya kuajiriwa mwezi Oktoba.
Aussems alipata dili la kuinoa Black Leopards FC msimu huu akiwa hana timu baada ya kuachana na Simba ambayo ipo chini ya Kocha Mkuu, Sven Vandenbroeck.
Kwa sasa inatajwa kuwa mikoba yake inaweza kuchukuliwa na kocha wa zamani wa Klabu ya Baroka FC Dylan Kerr.
Sababu ya kupigwa chini ndani ya timu hiyo inaelezwa kuwa ni matokeo mabovu ya timu hiyo kwa kuwa kwenye mechi tatu za mwanzo ameshindwa kupata ushindi.
Aliajiriwa na Black Leopards FC baada ya mabosi wa timu hiyo kuvutiwa na uwezo wake wakati akiifundisha timu ya Simba ambayo nayo ilimfuta kazi kwa kile ilichoeleza kuwa kushindwa kufikia malengo ambayo waliyaweka kimataifa kwa kutolewa mapema Ligi ya Mabingwa Afrika.
Akiwa ndani ya Simba SC aliweza kushinda taji la Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2018/19 na aliifikisha timu hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.