Vyanzo vya taarifa kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo vimethibitisha kuwa mwanamuziki maarufu nchini humo Élisabeth Tshala Muana Muidikay (Tshala Muana) amekamatwa.

Hadi kufikia sasa familia ya msanii huyo bado haijatoa taarifa yoyote lakini vyanzo vya habari nchini humo vinasema kwamba alikamatwa hapo jana majira ya mchana.

Hivi karibuni mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 62 alitoa wimbo uliofahamika kwa jina la ‘KUKOSA SHUKURANI’ ambao inaaminika kuwa chanzo cha matatizo yaliyomfika.

Mashairi ya wimbo huo yanaashiria mtu ambaye hakutajwa kwa jina alipewa mazingira mazuri yakumuwezesha maishani lakini amesahau kurejesha wema baada ya kuingia madarakani.

Wengi wanaamini kuwa mwanamuziki huyo ambaye ni mshindi wa tuzo mbalimbali anamzungumzia rais Felix Tshisekedi -lakini Tshala Muana bado hajathibitisha hilo.

Tshala Muana alikuwa karibu sana na familia ya aliyekuwa rais wa Congo Joseph Kabila.

De Bruyne: Kyle Walker hastahili lawama
Uchebe afungashiwa virago Black Leopards