Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema Serikali inatarajia kujenga kiwanda cha ukubwa wa kati cha kubangua Korosho, kuwawezesha wananchi kuzalisha mafuta kwa kutumia maganda ya korosho ili waweze kupata faida zaidi na kuifanya Lindi ifunguke kiuchumi.
Rais Samia amesema hayo wakati akihutubia wananchi wa Ruangwa katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Kilimahewa na kudai kuwa Serikali itaendeleza utafiti zaidi katika sekta ya madini ili kujua kiasi cha dhahabu kilichopo na kuwapanga velmimbaji wadogo wadogo ili wachimbe kitaalamu.
Aidha, mara baada ya kuweka jiwe la msingi la Barabara ya Ruangwa Nanganga (km 53.3) yenye thamani ya shilingi bilioni 50.3, Rais Samia alisema Serikali pia ina mpango wa kuunganisha Wilaya za Mkoa wa Lindi kwa Barabara zenye lami huku akiwataka Wananchi kuongeza uzalishaji wa mbaazi na ufuta.
Rais Samia pia alizungumza na wananchi wa vijiji vya Nanganga na Nandagala akiwa njiani kuelekea Lindi mjini na kuwasikiliza Viongozi mbalimbali katika mkutano uliofanyika Mtama Mkoani Lindi ikiwa ni muendelezo wa Ziara yake Mikoa ya Kusini.