Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Ureno, Marcelo Rebelo de Sousa juu ya uimarishwaji wa mahusiano yaliopo baina ya nchi hizi mbili kasa katika sekta ya uchumi wa buluu kwa kutumia rasilimali za Bahari.
Mazungumzo baina ya Makamu wa Rais Dkt. Mpango na Rais De Souza yamefanyika katika Ikulu ya nchi hiyo iliyopo jijini Lisbon nchini Ureno ambapo amemueleza azma ya Serikali katika kukuza uchumi wa buluu ikiwemo mikakati ya kutumia vema bahari na rasilimali zake.
Amesema Tanzania imejaliwa kuwa na ukanda mrefu wa pwani wa takribani kilomita 1,450 ambapo ukanda wa kiuchumi wa kipekee unafikia kilomita za mraba 223,000 hivyo ushirikiano baina ya mataifa hayo mawili utakua na manufaa.
Amesema, Tanzania imeweka mikakati ya kujenga Bandari ya uvuvi katika Bahari ya Hindi, ziwa Victoria na Tanganyika itakayochangia katika kuongeza mapato katika sekta hiyo.
Kwa upande wake, Rais wa Ureno, Marcelo Rebelo de Sousa amesema nchi yake ipo tayari kutoa ushirikiano katika ujenzi wa Bandari hiyo ya uvuvi itakayosaidia Tanzania kunufaika kupitia rasilimali za Bahari na kuimarisha uchumi huo wa buluu.
Rais Marcelo ameongeza kuwa, Ureno ipo tayari kushirikiana na kuhakikisha Tanzania inapiga hatua za kimaendeleo katika kukuza sekta ya biashara na uwekezaji.
Dkt. Mpango yupo nchini Ureno kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Pili wa Umoja wa Mataifa kuhusu Uhifadhi wa Bahari na Rasilimali zake, wenye lengo la kuhamasisha juhudi za Mataifa katika kufanikisha utekelezaji wa Lengo la 14 la Maendeleo Endelevu (SDG).