Serikali imewashauri Wazazi na Walezi kuwakatia Bima ya Afya watoto kwa ajili ya kuwaondolea gharama za matibabu pindi wanapopata maradhi mbalimbali.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu ameyasema hayo wakati akiongea na wananchi waliokua wakipata matibabu kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, General.

Amesema, kukamilika kwa mchakato wa sheria ya Bima ya Afya kwa wote, utasaidia wananchi wote kupata huduma zote za afya kuanzia ngazi ya msingi hadi Taifa ambapo kutawekwa kiwango nafuu.

“Bima ya afya kwa wote itamuwezesha mwananchi yeyote bila kujali hali yake ya maisha kutapata huduma za matibabu pamoja na vipimo kwenye vituo vya afya hadi ngazi ya Taifa,” amesema.

Aidha ameongeza kuwa Wizara ya Afya ipo katika hatua za mwisho za kupitisha sheria ya Bima ya Afya kwa wote na kiwango cha kulipia kwa mwaka kitakua ni nafuu ili kumuwezesha mtanzania kupata huduma zote kama anazopata mtumishi wa umma ikiwepo kulazwa na vipimo hadi Hospitali ya Taifa.

“Wakati tunasubiri Sheria ya Bima ya Afya kwa wote hivyo ni muhimu wazazi na walezi kuwakatia bima ya afya watoto wao kwa gharama ya 50,400 kwa mwaka na itamuwezesha kupata huduma hadi ngazi ya Taifa”.

Amesema, “Kwa sasa Bima hii sio lazima lakini nitakutana na wamiliki wa shule zote za Sekondari nchini katika kikao tutaweke takwa hili la kukata bima ya Afya kwa wanafunzi wa Sekondari.”

Hata hivyo, amesema Serikali imechukua hatua hiyo baada ya kuona watoto wakiugua mashuleni wanarudishwa nyumbani kwa ajili ya matibabu lakini uwepo wa bima utasaidia kupata matibabu popote.

Ameongeza kuwa, “Tunaanza hatua kwa hatua kama tulivyoanza kwenye vyuo vikuu kwa mwanafunzi kuwa na bima ya Afya ya NHIF na sasa kwa wanafunzi wa sekondari baada ya kuongea na wamiliki wa shule hizo na hata hii ya bima ya Afya kwa wote tumesema hatutawakamata watu kwamba ni lazima pia tunasubiri sheria ipitishwe.”

Utendaji Wakurugenzi, Wakuu wa idara kupimwa
Uchumi wa buluu watikisa anga Kimataifa