Jeshi la Polisi nchini limekamilisha uchunguzi wa awali wa tukio la kuuawa kwa watu wanne wakiwemo askari wake watatu lililotokea hivi karibuni mkoani Dar es Salaam, na kudai kuwa uchunguzi huo umethibitisha mhusika wa tukio hilo alikuwa ni gaidi.
Tukio lilitotokea Agosti 25 mwaka huu katika makutano ya barabara ya Kenyatta na Ali Hassan Mwinyi karibu na Ubalozi wa Ufaransa.
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini Camilius Wambura amewaeleza waandishi wa habari jijini Mwanza kuwa, mtuhumiwa wa tukio hilo Hamza Mohamed alikuwa ni gaidi aliyedhamiria kuleta madhara makubwa kwa vyombo vya ulinzi na usalama.
Aidha DCI Wambura amesema kuwa uchunguzi ulijikita katika mambo makuu matatu ambayo ni kutaka kutambua Hamza Mohammed ni nani, nini kilimsukuma Hamza kwenda kufanya tukio lile na kutaka kutambua mshiriki mwingine katika tukio hilo.
“Amekuwa akijifunza mambo mbalimbali kupitia mitandao ya kijamii ambayo kwa kipindi kirefu amekuwa akijifunza mambo ya kigaidi kwa kuangalia mitandao ambayo inaonyesha matendo ya Al-Shabab na makundi kama ISIS yanayoendelea na wagaidi wengi hujifunza kupitia mitandao hiyo,” Amesema Wambura.
Akizungumza kuhusiana na habari zilizoenea mtandaoni Kuhusu taarifa zinazodai kwamba Hamza aliwashambulia askari hao kwa sababu walimdhulumu madini yake, DCI amekanusha na kusema katika uchunguzi huo wamebaini kwamba Hamza hakuwa na madini wala fedha katika mazingira yale.