Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kupitia chuo cha Sayansi za Mawasiliano na Elimu Angavu, kimetengeneza mfumo wenye uwezo wa kuhakiki taarifa na hotuba mbalimbali na kubainisha kama ni halisi au zimechezewa na wahalifu wa kimtandao.

Mkuu wa Kitivo cha Elimu Ang’avu wa chuo hicho, Prof. Leonard Mselle amesema hayo Jijini Dar es Salaam katika mkutano uliowashirikisha wadau wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) juu ya utafiti wa masuala ya usalama wa mtandao uliofanywa na chuo hicho.

Profesa Mselle amesema mwaka 2013, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) walitoa tangazo la kushindana kuandika makala ambazo zitasaidia maendeleo ya ICT na chuo hicho kilishindana na moja ya mada ambazo waifanyia kazi ni masuala ya usalama wa mitandao.

“Tumeshafanya hiyo kazi na sasa ni mwaka wa tatu lakini mojawapo ya malengo ambayo tulisema tungewekeza katika huu utafiti ni kuweza sisi wenyewe kutengeneza mifumo au mitambo ambayo itahakikisha kwamba kuna usalama wa mitandao,” amesema Prof. Mselle

Amesema picha au sauti zinazochukuliwa zinaweza kuharibiwa na kupeleka ujumbe ambao ni tofauti kwa kutumia mifumo ya kidijitali hivyo wao wametengeneza mfumo ambao utaonesha kwamba taarifa hiyo, picha au sauti fulani imeharibiwa na siyo halali.

Hata hivyo, Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) inayochapisha magazeti ya Daily News, Sunday News, Habarileo na SpotiLeo, Dkt.  Jim Yonazi amesema suala la usalama wa mtandao ni jambo muhimu hasa kwa kuzingatia teknolojia inakua kila siku.

Kala Jeremiah: Jina Harmorapa ni kubwa kuliko baadhi ya majina ya wasanii wenye albamu mbili sokoni
Polisi 'watinga' nyumbani kwa Gwajima, mwenyewe afunguka