Kufuatia kusambaa kwa picha kadhaa kwenye mitandao ya kijamii, zikiwaonyesha wakuu wa nchi za Afrika akiwemo rais wa Kenya, William Ruto na rais wa Tanzania, Samia Suluhu wakisafirishwakwa basi kuelekea katika eneo la mazishi ya Malkia Elizabeth huko Westminster Abbey jijini London, ufafanuzi juu ya tukio hilo umetolewa.
Hatua hiyo, ilifuatia Viongozi wote wa kigeni kusafirishwa kwa makundi ndani ya mabasi, huku Rais wa Marekani, Joe Biden na mkewe Jill wakiruhusiwa kusafiri hadi kwenye ibada ya mazishi ya Malkia Elizabeth Jumatatu ya Septemba 19 kwa gari la limousine la kivita la rais maarufu kama “The Beast”.
Tozo hailengi kumpa mzigo Mwananchi: Mwigulu
Huku mazishi hayo, yakiongoza katika mitandao ya kijamii, kukiwa na hashtag juu ya maziko ya malkia Elizabeth II, inaonekana watumiaji wengi wa mitandao ya kijamii hawakufurahishwa na mpango huo wa kuwasafirisha Viongozi wa mataifa ya Afrika kwa mabasi, mpango ambao ulitangazwa siku chache kabla ya mazishi.
Wengine hata hivyo walikuwa na maoni tofauti ambapo baadhi yao walidai Marekani isingeweza kumruhusu rais wao kupanda basi kwani Interpol na FBI wasingekubali kwani Biden ni rais wa taifa lenye nguvu zaidi duniani hivyo usalama wake ulitakiwa kuwa wa juu zaidi huku wengine wakidai kitendo hicho ni dhihaka kwa Waafrika.
Kulingana na tovuti ya kituo cha Habari cha Express ya Uingereza, Ikulu ya White House ilimtaka Biden asafiri kwa kutumia msafara wa magari sita kutokana na sababu za kiusalama, ombi ambalo lilikubaliwa na maafisa wa Uingereza.
Chapisho hilo pia lilidai kuwa wageni wengine walisafirishwa kwa mabasi ili kupunguza msongamano wa magari na kwamba Biden si mtu pekee aliyetengwa na safari ya basi la VIP bali wengine ni pamoja na familia za kifalme kutoka nchi za Ulaya wakiwemo viongozi wa nchi za G7, kama Emmanuel Macron wa Ufaransa, Mfalme wa Japani Naruhito, na Justin Trudeau wa Canada.