Maelfu ya watu wameanza kuondolewa kwenye makaazi yao katika mji mkuu wa Ufilipino, Manila, baada ya mlima wa volcano wa Taal kuanza kurusha majivu na mawe angani.
Mamlaka ya utaalamu wa matetemeko ya ardhi nchini humo imeongeza kiwango cha hofu hadi nne chini ya tano ikisema kuwa kuna uwezekano wa volcano katika mlima huo kuripuka katika kipindi cha masaa au siku kadhaa zijazo.
Hadi wakaazi elfu nane walikuwa wameambiwa waondoke kutoka eneo hilo na kufikia jana jioni watu elfu sita walikuwa wametoka katika eneo lenye hatari.
Matetemeko madogo madogo ya ardhi tayari yamesikika katika maeneo yaliyo karibu na mlima huo.
Maafisa wa usafiri wa ndege wameamrisha kusitishwa kwa safari zote za ndege zinazoingia na kutoka katika mji mkuu wa Manila.
Maafisa wa serikali wametangaza kufungwa kwa shule Jumatatu na wakawaonya wakaazi kutoka nje.