Mamlaka ya Usafiri wa Anga nchini Uganda (UCAA), inatarajia kufungua uwanja wa kimataifa wa Entebbe na kuruhusu safari za ndani na nje, Kuanzia Oktoba 1, mwaka huu, baada ya miezi mitano ya kuzuia safari za ndege za abiria ili kudhibiti maambukizi ya Covid 19.
Hatua hiyo ni mfululizo wa jitihada za Serikali ya nchi hiyo chini ya rais Yoweri Museveni, kulegeza masharti, na kufufua uchumi ulioathirika vibaya kutokana na mlipuko wa ugonjwa huo.
Aidha mamlaka hiyo imesema kuwa ndege 13 zimeruhusiwa kuingia na kutoka kwa siku ya kwanza na 10 zitafanya safari siku ya pili.
Miongoni mwa mashirika yanayotarajiwa kufanya safari ni pamoja na Uganda Airlines, Air Tanzania, Kenya Airways, Emirates, RwandAir na KLM.