Tume inayosimamia mawasiliano nchini Uganda (UCC) imeandika barua kwa kampuni ya Marekani ya Google, ikiitaka kampuni hiyo ifunge stesheni kadhaa za televisheni zinazopeperusha matangazo yake kupitia You tube.
Kwamujibu wa kituo cha habari cha VOA, miongoni mwa stesheni hizo ni Ghetto TV, inayomilikiwa na chama cha National Unity Platform (NUP), cha mgombea wa urais Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine.
UCC imetaka takribani stesheni 13 zinazopeperusha matangazo yake moja kwa moja kupitia You tube, kufungwa kwa msingi kwamba zimekiuka sheria na maadili ya habari nchini humo.
“tume ya mawasiliano ya Uganda imepokea malalamiko kadhaa kutoka kwa maafisa wa serikali akiwemo waziri wa mambo ya ndani, mwenyekiti wa usalama wa taifa, polisi na jeshi la nchi hiyo kuhusu habari zinazopeperushwa na vituo hivyo vinavyotumia You tube na kwamba vinapeperusha habari ambazo zinavunja sheria ya mawasiliano ya Uganda, ya mwaka 2013 na sheria inayosimamia habari ya mwaka 2019, ibara ya 8 sehemu ya 2.” imeandika barua hiyo
Televisheni ambazo zimetajwa kwenye barua ya UCC ni pamoja na TMO Online, Lumbuye Fred, Trending Channel Ug, Uganda Yaffe, Uganda News Updates, Ghetto TV, Busesa Media Updates, Uganda Empya, Map Mediya TV, KK TV, Ekyooto TV, Namungo Media, JB Muwonge na Bobi Wine 2021.
Kulingana na ibara ya 27 ya sheria ya maudhui nchini Uganda, hakuna mtu anaruhusiwa kupeperusha habari bila ya kuwa na leseni ya tume ya mawasiliano ya nchi hiyo na anayefanya hivyo anaweza kuhukumiwa mwaka mmoja gerezani, kulipa faini au kulipa faini na kifungo cha mwaka mmoja gerezani.
“Kwa hivyo, kwa kuzingatia sheria ya mawasiliano ya mwaka 2013 namba 5(1) (b), (j), (x), 6 na 45, Tume inataka Google kufunga kabisa stesheni hizo,” inasema barua ya UCC kwa kampuni ya Google.