Umoja wa Mataifa (UN) umesema licha ya juhudi za kuzuia na kutibu ugonjwa wa kisukari bado idadi ya watu wanaougua ugonjwa huo inaongezeka kote duniani.
Wakati dunia ikiadhimisha siku ya kisukari leo Novemba 14, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema kuwa kinachotia hofu zaidi ni kuwa ongezeko la wagonjwa ni katika nchi za kipato cha chini na cha kati, ambazo hazina vifaa vya kutosha vya uchunguzi wa ugonjwa huo na dawa.
Shirika la afya la Umoja wa Mataifa (WHO), linatarajia kuzindua mkataba wa kimataifa dhidi ya Kisukari, ambao ni mpango mpya wa kusaidia kuweka muundo wa pamoja wa kupunguza mzigo utokanao na ugonjwa huo kwa mwaka ujao 2021.
Mwaka 2007 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio namba 61/255 likitangaza kuwa tarehe 14 mwezi Novemba kila mwaka iwe siku ya kisukari duniani.
Azimio hilo lilitambua udharura wa kuendeleza juhudi za kimataifa na kuboresha afya ya binadamu na kuhakikisha anapata huduma bora za afya na malezi dhidi ya ugonjwa wa Kisukari.
Zaidi ya watu Milioni 460 kwa sasa wanakadiriwa kuishi na ugonjwa wa kisukari ulimwenguni, na idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka hadi milioni 578 kufikia mwaka 2030.